HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI, 2015, YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ILIYOTOLEWA TAREHE 1 MACHI, 2015 KUHUSIANA NA MAUAJI YA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI
Mauaji ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi
Ndugu wananchi;
Nimesikitishwa sana na taarifa kuwa mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) yameibuka upya baada ya hali kuwa tulivu mwaka 2011. Mwaka jana (2014) yalitokea matukio 3 katika mikoa ya Mwanza, Tabora na Simiyu na mwaka huu limetokea tukio 1 mkoani Geita.
Lazima tulaani vikali mauaji ya ndugu zetu albino. Ni vitendo vya kinyama ambavyo havitegemewi kufanywa au kutokea katika jamii yeyote ya watu waliostaarabika, ya watu wanaomuabudu Mungu. Watu wenye ulemavu wa ngozi ni wanadamu wenzetu, wenye haki sawa ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yao kama walivyo wanadamu wengine. Hawastahili kufanyiwa wanayofanyiwa. Hawapaswi kuishi kwa hofu katika kijiji chao, mtaa wao au katika nchi yao. Jamii nzima na sisi sote mmoja mmoja na katika umoja wetu, tunao wajibu wa kuhakikisha usalama wa maisha yao na mali zao kama ilivyo kwa watu wengine wote.
Kwa kweli, mauaji ya albino ni jambo linalofedhehesha na kulidhalilisha taifa letu. Ni vitendo visivyovumilika. Hatuna budi sote kushikamana na kuhakikisha kuwa tunapambana nao kisawasawa na kuwashinda. Tusikubali kamwe wakaturudisha kule kubaya tulikokuwa zamani. Naungana na Chama cha Albino Tanzania kulaani ukatili huu na kutaka watu wote wanaojihusisha na ukatili huu wasakwe, wakamatwe, wafikishwe Mahakamani na kupewa adhabu kali inayowastahili wanapopatikana na hatia.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa wakati wote Serikali imelipa uzito mkubwa suala la kudhibiti na kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi au kukatwa baadhi ya viungo vyao wenyewe wakiwa hai. Tumefanya hivyo bila ya kuchoka tangu tukio la kwanza baada ya mimi kuingia madarakani Aprili 17, 2006 na miezi mitatu tu kule Nyahunge, Geita alipouawa Alfa Amon ambapo watuhumiwa 2 waliuawa na raia. Mwaka 2007 kulikuwa na matukio 7. Mwaka 2008 ndio ulikuwa mwaka mbaya sana walipouawa watu 18.
Kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wananchi mauaji yalipungua na kuwa 9 mwaka 2009. Mwaka 2010 kukawa na tukio 1 na mwaka 2011 hapakuwepo na tukio lolote. Mwaka 2012 kukawa na tukio 1, mwaka 2013 aliuawa mtu 1 na 2 kujeruhiwa. Mwaka 2014 waliuawa watu 3 na 2 kujeruhiwa, na Januari, 2015 kumetokea tukio 1 kule Geita.
Ndugu Wananchi;
Tangu mwaka 2006 mpaka 2015, watuhumiwa 139 wametiwa nguvuni, miongoni mwao wako watuhumiwa 16 wa matukio ya Desemba na Januari mwaka huu. Mashauri 35 yamefunguliwa mahakamani na kati ya hayo 10 bado yanaendelea na yapo katika hatua mbalimbali. Watuhumiwa 73 wameachiliwa na 15 wamepatikana na hatia. Kati ya hao waliopatikana na hatia 13 wamehukumiwa kifo na wawili wamepata kifungo cha miezi 6. Watuhumiwa kwa matukio sita bado wanasakwa.
Matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yametokea katika mikoa 10 kati ya mikoa 30 hapa nchini. Mikoa hiyo ni hii ifuatayo: Mwanza matukio 13, Kagera 6, Tabora 5, Geita 4, Mara 4, Kigoma 4, Simiyu 3, Shinyanga 2, Arusha 1 na Mbeya 1. Utaona matukio 41 kati ya 43 yametokea katika ukanda wa ziwa ambapo pia wanaongoza kwa mauaji ya vikongwe na wanawake kwa sababu za ushirikina.
Ndugu Wananchi;
Inawezekana kuwa matukio ya hivi karibuni yanaashiria kuwa uhalifu huu unataka kuibuka upya. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na Watanzania kwa jumla, kuwa hatutaacha hali iwe mbaya kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Tutatumia mbinu na maarifa tuliyoyatumia kukabili wimbi kubwa la mauaji lililokuwepo mwaka 2007 na 2008 na kwa sababu hiyo tukaweza kupunguza hadi kufikia kutokuwa na tukio lolote la mauaji mwaka 2011.
Tunachokiomba kutoka kwa wananchi ni ushirikiano na msaada wa kuwafichua watu wanaofanya vitendo vya mauaji na kukata viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi. Pia wasaidie kutoa taarifa kuhusu wanunuzi wa viungo hivyo na waganga wanaochochea mahitaji ya viungo vya albino. Ushirikiano wa wananchi wa wakati ule uliwezesha kupatikana kwa mafanikio niliyaeleza. Naamini safari hii tukifanya hivyo tutafanikiwa pia.
Ndugu Wananchi;
Kutokomeza kabisa matukio ya mauaji na ukataji wa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi ni jambo linalowezekana. Hata hivyo, litategemea watu kuacha imani za ushirikina. Imani potofu, ati kuwa mtu akiwa na kiungo cha mtu mwenye ulemavu wa ngozi atafanikiwa katika shughuli zake za biashara, uvuvi na uchimbaji wa madini ndicho kichocheo cha uovu wote huu unaoendelea. Ni ujinga ulioje kwa mtu kuamini kuwa mafanikio yake hayatategemea juhudi zake na maarifa yake bali kuwa na kiungo cha mwanadamu mwenzake mwenye ulemavu wa ngozi.
Nilisema katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi Machi, 2008 kwamba, kama kuwa na kiungo cha albino ndiko kutakakomfanya mtu kufanikiwa katika shughuli zake za kibiashara na kiuchumi basi ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi wangekuwa ndiyo matajiri wakubwa nchini na duniani. Maana wao sio tu wana viungo bali wana mwili mzima. Kwa sababu ya kuwepo imani hizi za hovyo, juhudi za kuelimisha jamii kuachana na imani hizi potofu ziongezwe. Naomba hili ndilo liwe jambo la msingi katika mapambano haya. Tukifanikiwa katika hili, matatizo yote haya yatakoma. Serikali na jamii haitalazimika kushughulikia mambo haya ambayo siyo tu ni fedheha hata kumsimulia mtu bali yanatisha na kusikitisha.
Ndugu Wananchi;
Wiki ijayo nitakutana na baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi. Nimekubali maombi yao ya kukutana nao ili niweze kusikiliza maoni yao na tubadilishane mawazo juu ya namna bora ya kumaliza tatizo hili. Mimi naamini kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na jamii utatuwezesha kutokomeza mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na kuliondolea taifa letu aibu hii.